Change Language: English

Pamoja na Imam Hussein AS kutoka Madina hadi Karbala

Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji warahmatullahi wabarakatuh. Karibuni kusikiliza sehemu hii ya 4 ya mfululizo wa kipindi hiki maalumu cha Muharram, kinachokujieni chini ya anuani ya "Pamoja na Imam Hussein (AS) kutoka Madina hadi Karbala." Katika kipindi chetu hiki tutadondoa baadhi ya hotuba za Imam alizotoa mbele ya jeshi la Hur na pia maneno ya mtukufu huyo aliyowaambia masahaba zake Siku ya Ashura pamoja na jeshi la adui. Ni matumaini yangu kuwa mtanufaika na yale mtakayoyasikia katika kipindi hiki.

Kuwaonyesha uongofu, kuwaelimisha, kuwakamilishia hoja na kuondoa dhima kwa watu waliokuwa wameghafilika, ilikuwa ndio mbinu aliyoitumia Imam Hussein (AS) kila wakati na kila mahala alipopata fursa mwafaka ya kufanya hivyo. Akiwa amezingirwa na jeshi la Hur la askari elfu moja na katika lahadha ambapo hatari ilikuwa mbele ya macho yake, Imam aliuona wakati huo kuwa ni fursa mwafaka ya kutoa hotuba kwa watu. Kwa hotuba hiyo ya kusisimua ya Imam Hussein (AS) iliyokuwa imejaa fasaha na balagha, kama kulikuwa na shaka yoyote iliyosalia ingeondoka, na kama kulikuwepo na moyo wowote ulio tayari kuikubali haki basi ungeathirika. Imam Hussein aliianza hivi hotuba yake hiyo kwa kunukuu hadithi kutoka kwa babu yake mtukufu, Bwana Mtume Muhammad (SAW): Aliyoyasema ni haya: "Enyi watu, Mtume wa Mwenyezi Mungu SAW amesema: Muislamu yeyote atakayemwona Mfalme jeuri anayehalalisha aliyoharamisha Mwenyezi Mungu, mwenye kuvunja ahadi za Mwenyezi Mungu, anayezipinga na kuzipiga vita sheria na Sunna za Mtume na akawa anawafanyia waja wa Mwenyezi Mungu madhambi na uadui, lakini Muislamu huyo asisimame kukabiliana naye kwa vitendo au kwa maneno, basi ni juu ya Mwenyezi Mungu kumwacha mtu huyo aliyenyamazia hayo katika hali hiyo hiyo ya uovu na kumuingiza kwenye moto wa Jahannamu. Enyi watu! tambueni kwamba Bani Umayyah wameacha kumtii Mwenyezi Mungu na kujiwajibishia kumfuata shetani, wameeneza maovu na ufisadi na wameipindua mipaka ya Mwenyezi Mungu. Na mimi ni mstahiki zaidi wa kuongoza jamii ya Waislamu kuliko waovu hawa walioipindua dini ya Mwenyezi Mungu. Na mbali ya hayo, barua kutoka kwenu zilizonifikia na wajumbe wenu mliowatuma ni ushahidi kwamba mumenibai na kufunga ahadi nami kuwa hamtoniacha peke yangu mbele ya adui....kwa hivyo kama mngali mmeshikamana nayo na kuiheshimu ahadi hii basi mmeifikia nusra na uokovu. Mimi ni Hussein, Ibn Ali (AS) na mwana wa Fatima binti wa Mtume wa Mwenyezi Mungu. Nafsi yangu na zenu nyinyi Waislamu zimechanganyika pamoja, na watoto na familia zenu ni sawa na watoto wangu na familia yangu. Mimi ni kiongozi kwenu. Lakini kama hamtofanya hivyo na mkavunja ahadi yenu na mkaiacha bai'a yenu haitokuwa mara ya kwanza kufanya hivyo, kwani kabla yake mlimfanyia vivi hivi baba yangu, kaka yangu na mwana wa ami yangu Muslim... Nyinyi ni watu mlioiharibu fursa yenu kwa kufuata upotofu, na kila mwenye kuvunja ahadi, anafanya hivyo kwa hasara yake mwenyewe, nami ni mwenye kutumai kuwa Mwenyezi Mungu atanifanya nisiwe mhitaji kwenu."

Hotuba hiyo ya kusisimua na ya kutaalamisha ya Hussein Ibn Ali (AS) ilikuwa ya kukamilisha hoja na kuondoa dhima, na ya kuwalingania askari zaidi ya elfu moja ambao walishirikiana na Hur kumfungia njia Imam. Kuna nukta na vipengele kadhaa vya aina yake vinavyoonekana ndani ya hotuba hiyo. Kutumia na kutegemea maneno ya Mtume SAW katika kutaja sifa za utawala wa Bani Umayyah, kubainisha nafasi ya Imam, kufafanua sababu za harakati na mapambano yake, kuwatambulisha watu aina ya uhusiano wa Imam na jamii na kuweka wazi matarajio ya mustakabali wa harakati hiyo ni miongoni mwa nukta zilizokuwemo ndani ya hotuba hiyo.

Msafara wa Imam Hussein (AS) uliwasili Karbala katika siku ya pili ya mwezi wa Muharram. Katika ardhi hiyo, Imam, watu wa nyumba yake pamoja na masahaba zake walikabiliwa na hali ngumu isiyoelezeka. Adui alimfungia maji Imam, watu wa nyumba yake na masahaba zake ili labda aweze kuwavunja moyo na kudhoofisha istiqama yao; lakini ni katika hali na mazingira hayo kulishuhudiwa kujitolea mhanga kusio na kifani ambako hakujawahi kuonekana katika historia.

Imam Hussein (AS) alikuwa akijua vyema kwamba unahitajika moyo mkubwa kwa mtu kuweza kuvumilia masaibu na mambo makubwa yaliyokuwa yakimkabili yeye na watu wake na kusimama imara katika medani ya mapambano. Na ndiyo maana aliitumia fursa ya kila mahala na wakati kuzijenga na kuzifanya imara zaidi imani za wafuasi wake, harakati ambayo ilifikia kilele chake katika usiku wa kuamkia Ashura. Usiku wa kuamkia siku ya Ashura ulikuwa usiku wenye adhama kubwa zaidi na msisimiko mkubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia. Katika usiku huo Imam Hussein aliwakusanya wafuasi wake wote, na kwa mara ya mwisho akawatangazia bayana kwa kuwaambia: "Wakati wa kufa shahidi umewadia, na mimi ninaiondoa bai'a mliyonipa; akitumie kiza cha usiku kila anayehisi kuwa hatoweza kuandamana nami katika mapambano haya hapo kesho ashike njia na kuelekea kwenye maskani na mji wake." Kwa hakika ushauri huo wa Imam ulikuwa ndio mtihani wa mwisho aliowafanyia wafuasi wake. Matokeo ya mtihani huo yalikuwa ni radiamali na hisia za hamasa kubwa za masahaba wa mtukufu huYo ambao waliufuzu mtihani huo kwa kila mmoja na kwa namna yake alipodhihirisha uaminifu wake kwa Imam Hussein na kutangaza bayana kwamba atasimama imara na kubaki pamoja Imam hadi pumzi ya mwisho ya uhai wake.

MUZIKI

Alfajiri ya kuamkia siku ya Ashura na baada ya kusali Sala ya Asubuhi, Imam Hussein alisimama na kutoa hotuba iliyokuwa na msisimko na adhama isiyo na kifani, hotuba ambayo iliweka wazi sababu na pia matokeo ya subira na istiqama yao. Imam alisema:" Enyi mliotoka kwenye mifupa ya watu watukufu, kuweni na subira na uvumilivu, kwani mauti si kitu kingine ila ni daraja na kivuko cha kutoka kwenye tabu na mateso na kukufikisheni kwenye Pepo isiyo na mipaka na neema za milele. Ni nani kati yenu asiyefurahi kuondolewa kwenye gereza na kupelekwa kwenye kasri. Mauti haya haya kwa maadui zenu ni kuondoka kwenye kasri na kuelekea kwenye mateso".

Chimbuko la itikadi hiyo lilikuwa ni imani ya kweli juu ya Mwenyezi Mungu na matunda ya subira na istiqama. Baada ya hapo Imam Hussein aliwapanga wapiganaji wake. Kisha akalitupia jicho jeshi la kubwa la adui, na baada ya hapo akamuelekea Mola na kuanza kutaaradhia hali yake kwa kusema:"Ewe Mola! Wewe ndiye tegemeo langu katika wakati wa tabu na machungu, na wewe ndie tumaini langu wakati wa matukio ya kuhuzunisha na wewe ndie tegemeo langu katika matatizo. Katika lahadha hii ngumu ninashtakia hali yangu kwako wewe tu na nimeondoa matumaini kwa wengineo; ni wewe ndiye mwenye kunijua hali yangu na mwenye kuyaondoa mawingu ya majonzi na kunifikisha kwenye pwani ya utulivu." Katika munajati huo wenye adhama na wa kushtakia hali katika alfajiri hiyo ya kipekee, mtu anaweza kubaini na kumaizi sababu ya muqawama, subira na istiqama ya Imam Hussein (AS) pamoja na wafuasi wake. Naam, kumwamini na kumtegemea Mwenyezi Mungu huyafanya mazito na magumu kuwa mepesi, na humpa mja uwezo wa kuvumilia dhoruba zenye kuvunja miamba.

Hussein Ibn Ali (AS) aliwaona maadui wamejiweka tayari na kujizatiti barabara wakisubiri kupewa ishara ndogo tu ili waanzishe vita mpaka wakafikia hadi ya kumzuilia maji mtukufu huyo pamoja na wote alikuwa nao katika kambi yake wakiwemo wanawake na watoto wadogo. Katika hali na mazingira hayo sio tu Imam Hussein hakuwa tayari kuanzisha vita bali alitaka kuhakikisha anaitumia fursa kadiri inavyowezekana kulipa nasaha na mawaidha jeshi hilo la adui ili kwa upande mmoja njia ya haki na fadhila ipambanuke na ile ya batili, na kwa upande mwengine isije pengine wakawepo watu ambao kwa sababu ya kutokuwa na uelewa na kutotambua hakika ya mambo wakashiriki katika kumwaga damu ya Imam wa haki, na matokeo yake yakawa ni kutumbukia kwenye lindi la hilaki na maangamizi. Baada ya kuzipanga safu za wapiganaji wake, Imam Hussein (AS) alimpanda farasi wake, akampeleka shoti kwa masafa kutoka kwenye mahema ya kambi yake, na kwa sauti ya juu iliyosikika kwa uwazi kabisa akalielekea jeshi la Omar Saad na kulihutubu kwa kusema:

"Enyi watu! Sikilizeni maneno yangu na wala msifanye pupa ya kuanzisha vita na kumwaga damu, bali niacheni nitekeleze jukumu langu ambalo ni kukupeni nasaha na mawaidha na kubainisha sababu ya safari yangu. Ikiwa mtazikubali hoja zangu na mkafuata njia ya insafu pamoja na nami mtakuwa mmeifikia njia ya saada na wala hamtokuwa na sababu ya kuanzisha vita; la kama hamtozikubali hoja zangu na kutofuata njia ya insafu basi unganeni pamoja mtekeleze uamuzi na fikra yoyote batili mliyonayo kuhusiana na mimi na wala msinipe muhula. Lakini kwa vyovyote vile kusiwepo na kilichofichika kwenu katika jambo hili. Msaidizi na wa kuninusuru mimi ni Mwenyezi Mungu, ambaye ameiteremsha Qur'ani na Yeye ndiye mwenye kuwanusuru waja wema".

Naam, hivi ndivyo ulivyo moyo wa huruma na upendo wa Imam na kiongozi wa dini mwenye kuwapenda watu, ambaye hasiti hata kwa lahadha ndogo kufuata mwongozo alioainishiwa na Mwenyezi Mungu wakati alipokabiliwa na adui mwenye kiu ya damu yake. Hotuba hizo, nasaha na miongozo yote hiyo ilitolewa na Imam Hussein (AS) mara kwa mara katika siku ya Ashura, licha ya dhiki iliyokuwepo ya muda na wakati wa kufanya hivyo. Katika hotuba yake kwa jeshi la Omar Saad, Imam Hussein aliwatanabahisha wao na watu wa Kufa kwamba wasidhani kuwa anawaeleza hayo kwa lengo la kutaka mapatano na maridhiano, bali lengo la kufanya hivyo ni kutimiza hoja na kuondoa dhima, na kubainisha uhakika wa mambo ambao kutokana na nafasi yake ya Uimamu na jukumu la uongozi na la kufikisha uongofu alikuwa hana budi kuwafikishia wao uhakika huo.