Change Language: English

MSIMAMO WA AHLUL BAYT (A)

Maimamu wa Ahlul Bayt (a) walipinga njama hizi khabithi za kibani Umayya na mbinu zao za kishetani na walisimama kidete kwa nguvu zote walizokuwa nazo, kupambana na vimbi hili hatari na bida’ mbaya kabisa. Maimamu wa Ahlul Bayt (a) walitangaza kwa sauti kubwa mtu kujiepusha kushukulikia haja zake siku ya Ashura, na kugoma kufanya kazi siku hiyo na kuifanya kuwa ni siku ya huzuni na kulia na kumshutumu yule anayeitazama kuwa ni siku ya Baraka na kumuombea afufuliwe Siku ya Kiyama pamoja na wazushi wa bida’a hii ya kishetani ambao ni Banu Umayyah na wafuasi wao. Amri kutoka kwa Maimamu kuhusu kuweka msiba siku ya Ashura kwa kulia na kuamrisha wanafamilia kulia na kukutana kwa kulia… ni amri zilizotiliwa mkazo ambapo Imam anampa dhamana anayetekeleza hilo pepo. Kinyume na madai ya kuwepo baraka kwa kuweka na kununua chakula cha mwaka mzima siku ya Ashura, Maimamu wa Ahlul Bayt (a) wanalaani na kufichua njama za mti uliolaaniwa (Bani Umayyah) na wanazuoni wao. Lengo hasa la maadui hawa wa kizazi cha Mtume (s) ni kuwapotosha watu na kufunika tukio la huzuni na unyama walioufanya kwa kumuua kikatili Bwana wa vijana wa peponi, Imam Husayni (a), kipenzi cha Mtume (s) na hivyo kuepuka lawama na laana za Waislamu kwa kuwashughulisha na sherehe na kutabaruku. Waislamu kuliko kuhuzunika na kulia kama walivyofanya Mtume (s), watu wa nyumba yake, masahaba wema na Waislamu kwa kifo cha Imam Husayn (a), (bali pia mbingu na ardhi na vilivyomo vililia kwa msiba huu adhimu), wanasheherekea na kufurahi kwa kufuata uzushi wa Bani Umayyah! Mwenyezi Mungu apige mhuri nyuso zao kama alivyopiga nyoyo zao. BAADHI YA RIWAYA KUTOKA KWA MAIMAMU WA AHLUL BAYT i. Ibn Tawuus kama ilivyopokelewa kutoka kwa Imam Ridhwa (a) kwamba alisema: “Yeyote atakayeacha kushughulikia haja zake siku ya Ashura, basi Allah atamkidhia haja zake za Dunia na Akhera. Yeyote ambaye siku ya Ashura itakuwa ni siku ya msiba wake, huzuni na kulia, Allah atamjalia Siku ya Kiyama kuwa siku ya furaha yake na macho yake yatafurahi kuwa pamoja nasi Peponi. Na yeyote atakayeita siku ya Ashura kuwa ni siku ya Baraka na akaweka akiba kwa ajili ya familia yake, basi atambue hatabarikiwa katika alichokiweka na Siku ya Kiyama atafufuliwa na Yazid bin Muawiya na Ubaydullah bin Ziyad na Umar bin Saad, Allah awalaani katika sehemu ya chini kabisa Motoni. ii. At-Tuusiy: kutoka kwa Alqamah, kutoka kwa Abu Ja’far (a), katika hadithi ya ziyara ya Imam Husayn (a) siku ya Ashura kwa karibu au mbali, alisema: kisha amuomboleze Husayn (a) na kumlilia na awaamrishe waliomo ndani ya nyumba yake, ambao hana hofu nao, kulia na kuweka msiba ndani ya nyumba yake kwa kudhihirisha huzuni juu yake. Na wapeane pole kwa msiba wao wa Husayn (a) na ikiwa wakifanya hivyo, basi mimi nawapa dhamana kwa Allah ya malipo sawa na hijja elfu mbili, umra elfu mbili, na ghazwa (vita vya jihadi) elfu mbili. Nikasema: Wewe ni mwenye kuwadhamini hilo na msimamizi? Akajibu: mimi ni mdhamini na msimamizi kwa yule atakayefanya hivyo. Nikasema: na ni vipi tutakavyopeana pole? Akajibu: waseme: Allah aufanye ujira wetu na wa kwenu kuwa mkubwa kwa msiba wetu wa Imam Husayn (a), atujaalie sisi na nyinyi kuwa miongoni mwa wenye kulipiza kisasi chake pamoja na waliy wa Allah Imam Mahdi (a) kutoka kizazi cha Mtukufu Mtume (s). Na ikiwa utaweza, basi siku hiyo usishughulike kwa haja yoyote ile. Siku hiyo ni siku ya nuksi, haja ya muumini haikidhiwi, na ikikidhiwa basi haibarikiwi na hataona ndani yake uongofu. Pia asiweke akiba kwa ajili ya nyumba yake chochote kile, kwa sababu atakayefanya hivyo siku hiyo, hatabarikiwa katika alichokiweka na pia hatobarikiwa katika ahli zake. Basi wakitekeleza hayo, Allah atawalipa thawabu za hijja elfu moja na umra elfu moja na ghazwa elfu moja zote pamoja na Mtume (s). Atakuwa na ujira na thawabu za kila nabii na rasul na wasiy na siddiqi na shahidi ambaye alikufa au aliuawa toka siku Allah aliiumba dunia hadi Siku ya Kiyama. iii. As-Suduuq: kutoka kwa Jublah al-Makkiyyah, ambaye anasimulia kwamba: “Nilimsikia Maytham at-Tammaar (r) akisema: Wallahi Ummah huu utamuua mtoto wa nabii wake katika Muharram tarehe 10, na maadui wa Allah wataifanya siku hiyo ni siku ya Baraka, na hilo lipo limetangulia katika elimu yake Allah. Hilo nalifahamu kwa maarifa aliyonikabidhi bwana wangu Amiri wa waumini (Imam Ali). Alinipa habari kwamba kila kitu kitamlilia hata wanyama maporini, samaki majini, na ndege angani. Ataliliwa na jua, mwezi na nyota, mbingu na ardhi, waumini binadamu na majini, malaika wote wa mbinguni na ardhini, Ridhwan na Malik na wenye kubeba Arshi. Mbingu itanyesha damu na majivu. Kisha akasema: wamelaniwa wauaji wa Imam Husayn (a) kama walivyolaaniwa washirikina wanaomwabudu mungu mwingine pamoja na Allah na kama walivyolaaniwa mayahudi na manasara na Majusi.” Jublah akamuuliza: Ni vipi ewe Maytham watu siku kama hiyo ya kuuliwa Husayn (a) wataifanya kuwa ni siku ya baraka!!! Maytham (r) akalia kisha akasema: Watadai hilo kwa hadithi watakayozusha kwamba siku hiyo ni siku ambayo Allah alimsamehe Adam (a) ilhali ya kuwa Adam (a) alisamehewa katika Dhulhijjah, pia watadai kwamba ni siku Allah alikubali toba ya Daudi (a), ilhali ya kuwa toba ya Daudi ilikubaliwa katika Dhulhijjah, pia watadai kwamba ni siku Allah alimuokoa Yunus (a) kutoka tumboni mwa papa, ilhali ya kuwa Allah alimuokoa Yunus (a) katika Dhulhijjah, pia watadai ya kwamba ni siku ambayo safina ya Nuh (a) iliweka nanga kwenye mlima Judiy, ilhali ya kuwa safina iliweka nanga tarehe 18 Dhulhijjah, pia watadai ya kuwa ni siku ambayo Allah alipasua bahari kwa ajili ya Bani Israil, na ilhali ya kuwa hilo lilikuwa katika Rabiul-Awwal. Kisha Maytham akasema: ewe Jublah fahamu ya kwamba Husayn bin Ali (a) ni bwana wa mashahidi Siku ya Kiyama, na masahaba wake ni wenye daraja juu ya mashahidi wengine. Ewe Jublah! Siku utakapoona mbingu (jua) ni nyekundu kama vile damu mbichi basi elewa ya kwamba bwana wa mashahidi Imam Husayn (a) ameuliwa. Jublah anasimulia: siku hiyo nilitoka na kuona jua kwenye vyambazi ni kama vile shuka zilizopakwa rangi nyekundu, nikapiga kelele na kulia na kusema: Wallahi amekwishauliwa bwana wetu Husayn bin Ali (a).” iv. Zurarah alisema: Abu Abdillah (a) alisema: “Ewe Zurarah hakika mbingu ilimlilia Husayn (a) asubuhi arobaini kwa damu, na Ardhi ililia asubuhi arobaini kwa weusi, na jua lilimlilia asubuhi arobaini kwa kupatwa (kusuf) na wekundu, na milima ilipasuka na kupukutika, na bahari zilichafuka, na malaika walimlilia Husayn (a) asubuhi arobaini, na hakuna mwanamke atokanaye nasi ambaye alipaka rangi wala kupaka mafuta wala wanja wala kuchana nywele hadi pindi tulipoletewa kichwa cha Ubaydullah bin Ziyad (Allah amlaani) na bado tunaendelea kuwa ndani ya mazingatio baada yake…” v. Sudduq: ‘Abdullah bin Fadhl al Hashimiy anasema: “Nilimwambia Imam Ja’far Sadiq (s): Ewe mtoto wa Mtume (s), ni vipi siku ya Ashura iligeuka kuwa siku ya msiba na huzuni na kilio kinyume cha siku aliyofariki Mtume (s) na siku aliyofariki Bibi Fatima (a) na siku aliyouliwa Imam Ali (a), na siku aliyouliwa Imam Hasan (a) kwa sumu? Akajibu kwa kusema: Siku ya Husayn (a) ni siku ya msiba mkubwa kuliko siku zingine zote, na hiyo ni kwa sababu ‘As-habul Kisaa’ ambao walikuwa ndiyo wabora wa viumbe vyote kwa Allah walikuwa ni watano. Alipoondoka Mtume (s) walibaki Ali, Fatima, Hasan na Husayn. Watu wakipata faraja kwao kwa msiba huo. Alipofariki Fatima (a), ikawa faraja ni kwa Ali, Hasan na Husayn, na alipofariki Ali (a), faraja ikabaki ni kwa Hasan na Husayn, na alpofariki Hasan (a), ikawa faraja ni kwa Husayn (a) peke yake. Alipouliwa Husayn (a) hakuna aliyekuwa amebaki miongoni mwa Ahlul-Kisaa ili awe ni faraja kwa watu. Kuondoka kwake ilikuwa ni sawa na kuondoka kwa wote pamoja. Kwa sababu hiyo msiba wake ni mkubwa zaidi. Abdullah bin Fadhl al-Hashimy akauliza tena: Ewe mtoto wa Mtume! ni kwa nini watu hawakuwa na faraja kwa Imam Ali Zaynul-Abidin (a) kama walivyokuwa na faraja katika baba zake? Imam Akajibu: bila shaka Ali Zaynul-Abidin (a) ni Imam na hujja kwa walimwengu baada ya baba zake lakini yeye hakuwahi kukutana na Mtume (s) na kupata mafunzo kutoka kwake. Elimu yake ni urithi kutoka kwa baba yake hadi kwa Mtume (s), ama Imam Ali (a), Fatima (a), Hasan (a) na Husayn (a), watu waliwaona kwa kipindi wakiwa pamoja na Mtume (a) katika hali mbalimbali. Kwa hivyo wakawa kila wakimwangalia kila mmoja miongoni mwao, wanakumbuka hali yake pamoja na Mtume na kauli ya Mtume (s) kwake na kuhusu yeye. Walipofariki, watu walipoteza kuwaona watukufu hawa. Na ile hali ya kuwakosa wote haikujitokeza kwa yeyote miongoni mwao ila alipofariki Husayn (a), na kwa sababu hiyo ndiyo msiba wake ukawa ni adhimu. Abdullah bin Fadhl anasema: nilimuuliza ewe mtoto wa Mtume (s) ni vipi Waislamu wakaita siku ya Ashura kuwa ni siku ya Baraka? Akalia, kisha akasema: Alipouliwa Imam Husayn (a), watu walielekea Sham kwa Yazid na wakazusha kwa ajili yake hadithi na wakapewa malipo ya mapesa. Miongoni mwa waliyoyazusha kwa ajili yake ni suala la siku hii, kwamba ni siku ya Baraka ili watu wajiepushe na kilio na msiba na kuifanya kuwa ni siku ya faraja na furaha na kutabarruku na kujiandaa…. Allah ahukumu baina yetu na wao.