Change Language: English

Mshauri wa mufti wa Misri: Imam Hussein AS aliuawa na watu waliokuwa na fikra za kitakfiri

Mshauri wa Mufti wa Misri, Majd Ashur amesema kuwa, Imam Huseein AS, mjukuu wa Mtume Muhammad SAW aliuliwa shahidi na watu waliokuwa na fikra za kigaidi na kitakfiri.

Ashur ambaye pia ni katibu wa fatwa katika ofisi ya Darul-Fatwa ya nchi hiyo, ameyasema hayo leo mjini Cairo, ambapo sambamba na kukosoa vikali fikra hizo za kuwakufurisha Waislamu wengine ambazo pia ni sawa na fikra lilizokuwa nazo kundi potofu la Makhawarij, mwanzoni mwa kudhihiri Uislamu, amesema kuwa, Imam Hussein AS aliuliwa kwenye jangwa la Karbala, Iraq na watu wenye fikra hizo. Aidha ameongeza kuwa, mtukufu Mtume Muhammad SAW aliwaonya sana Waislamu juu ya kudhihiri makundi ya watu wenye misimamo mikali ambayo inakinzana na mafundisho ya dini tukufu ya Uislamu. Mwanafikra huyo wa Kiislamu nchini Misri, amegusia pia tuhuma kali zinazotolewa na baadhi ya televisheni na mitandao ya kijamii na magazeti dhidi ya Waislamu wa Kishia, na kusema kuwa maadhimisho ya kumbukumbu za ukatili waliofanyiwa Imam Hussein AS na watu wa familia ya Mtume ambazo hufanywa na Waislamu wa Kishia huwa hazina nia ya kumshirikisha Mwenyezi Mungu. Majdi Ashur ameyasema hayo wakati wa maadhimisho ya kumbukumbu za kufikishwa kichwa cha Imam Hussein mjini Cairo, baada ya mauaji ya Karbalaa, zaidi ya miaka 1370 iliyopita, maadhimisho ambayo hufanyika kila mwaka nchini Misri.