HOTUBA YA AL-USTADH SHEIKH ABDULLAH IBN SALEH AL-FARSI ALIYOITOA KWENYE HAFLA YA KUKUMBUKA MAUAJI YA IMAM HUSAIN BIN ALI (A.S) – ZANZIBAR 1361 A.H 1942 A.D
Enyi wageni waheshimiwa na nyote mliohudhuria.
Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema Mwenye kurehemu. Sifa zote njema anastahiki kusifiwa Mwenyezi Mungu Mola wa walimwengu. Kisha sala na salamu zimshukie mbora wa Mitume na Manabii, Bwana wetu Muhammad aliyemuaminifu na pia ziwashukie kizazi chake ambao Mwenyezi Mungu amewaondolea uchafu na kuwatakasa mno.
Ama baada hayo, kwa hakika kamati iliyoandaa kumbukumbu hii ya mauaji ya Imam Husain a.s ilikuwa imemtaka mwalimu wangu Al-Allamah Sheikh Abubakar Ibn Abdillah Bakathir aje asimame kwenye mahafali hii tukufu ili azungumzie japo kidogo tu kuhusu tukio hili kubwa lililotokea Karbala. Tukio ambalo hapana shaka japo nila siku nyingi lakini haliwi kongwe wala uchungu wake hausahauliki pamoja na kupitiwa na miezi mingi na miaka mingi.
Kwa kuwa siku hizi afya ya Sheikh siyo nzuri ameniteuwa nimuwakilishe mahala hapa japo kuwa mimi si miongoni mwa watu wa rika lake wala siko kati ya watu wenye ufasaha wa kiwango chake.
Hapana shaka kwamba yeye alikuwa ndiyo mwenye kustahiki mno mahala hapa, lakini maamuzi ya Mwenyezi Mungu ndiyo yenye kupita pindi yanapo mfika mtu basi huwa hana njia ya kuyaepuka.
Na ilivyokuwa kuna mawaidha na mazingatio katika kumbukumbu za misiba, tumeona ni vema tueleze mawaidha na mazingatio yaliyomo ndani ya msiba huu mkubwa uliotukusanya katika usiku huu ili tuuhuishe.
Kwa hiyo mimi nasema kwamba, “Kwa hakika mauaji ya Imam Husain a.s ni miongoni mwa matukio makuwa yenye kusikitisha na kuhuzunisha, lakini makumbusho yake ni yenye manufaa japokuwa hadithi yake inamtia huzuni kila Muislamu na kumchukiza kila mwenye akili.”
Huenda Mtu asiye jua kitu kuhusu mwenendo wa Mwenyezi Mungu kwa ujumbe wake akasema, “Ni kwa nini basi Mwenyezi Mungu hawasaidii watu wa haki dhidi ya maadui wao ambao wako kwenye upotovu bila hata ya wao kunyanyua panga zao (dhidi ya madui hao) wala bila mapambano ya mikuki?”
Sisi tutamjibu kwa kusema kuwa,”Hatuna shaka yoyote ndani ya nyoyo zetu kwamba, Mwenyezi Mungu hawasaidii watu hao wa haki bila mapambano ili tu apate kuwapambanua wale walioamini na wengine awafanye kuwa ni Mashahidi miongoni mwao, kama alivyosema Mwenyezi Mungu ndani ya Sura Al-Imran, “Ili Mwenyezi Mungu apambanuwe wale walioamini na awafanye miongoni mwao kuwa ni mashahidi na Mwenyezi Mungu hawapendi madhalimu, na ili Mwenyezi Mungu awasafishe walioamini na kuwafuta waliokufuru” Na vile vile aliposema ndani ya Suratul Baqarah, “Mnadhani kuwa mtaingia peponi na hali hamjajiwa na mifano (wa yale yaliyowajia) wale waliopita kabla yenu? Yaliwapata mashaka na madhara na wakatetemeshwa mno hata Mtume na wale walioamini pamoja naye wakasema, “Msaada wa Mwenyezi Mungu utafika lini? Jueni kuwa msaada wa Mwenyezi Mungu uko karibu.” 2:214
Mawaidha na mazingatio yanayotokana na mauaji ya Imam Husain (a.s)
Hapana shaka kwamba hapo kabla nilikuahidini kwamba, nitakuelezeni baadhi ya mawaidha na mazingatio yaliyomo ndani ya tukio la mauaji ya Imam Husain a.s, kwa hiyo sasa hivi nitawaeleza kile nilichokuwa nimekiahidi kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu na ninasema:
Kwanza: Imam Husain a.s ndiyo mtu wa kwanza aliyeuonesha Umma njia ya kutoka dhidi ya watawala waovu na wajeuri na akaulingania (Umma) kupinga dhulma kwa kila mwenye uwezo wa kulifanya hilo. Hivyo basi aliitoa nafsi yake na akajitolea damu yake ili kusimamisha haki, uadilifu na Sunna ya Mtume s.a.w dhidi ya maovu, ubinafsi na kulewa madaraka.
Hapana shaka kwamba babu yake s.a.w amesema, “Yeyote atakayeanzisha mwenendo mzuri basi atapata ujira wake na ujira wa wale watakaoutumia mwenendo huo” Nampa hongera Imam huyu kwa kuweka mwenendo huu mzuri.
Pili: kitendo hicho cha Imam Husain a.s kilikuwa ni cha kuwatia nguvu na kuwapa moyo wa kujituma wale wote ambao wanapata matatizo katika kutumikia dini ya Mwenyezi Mungu ili wasije wakajiona kuwa pengine wanapatwa na matatizo hayo kwa sababu labda wao ni wanyonge na ni watu dhalili mbele ya Mwenyezi Mungu, au labda wakahisi kuwa wao wako kwenye batili na maadui zao ndiyo walio kwenye haki kwa hayo wayatendayo, na kwa ajili hii wakavunjika nguvu na kuacha msimamo wao. Lakini iwapo tu watamkumbuka Imam Husain a.s. na misiba iliyompata hali ya kuwa yeye alikuwa akitetea haki na maadui zake wakitetea batili, basi hapo watu wema hujirudi kutokana na dhana ile potofu, kwani watu wengi hufikia hali aliyoisema MwenyeziMungu katika Suratul-ankabut. “Na miongoni mwao wako wanaosema, tumemwamini Mwenyezi Mungu, lakini wanapoudhiwa katika njia ya Mwenyezi Mungu huvifanya vituko vile vinavyowakuta toka kwa watu kama kwamba ni adhabu ya Mwenyezi Mungu.”
Tatu: Tukio la kujitoa Muhanga Imam Husain a.s liwe ni mazingatio kwa yeyote yule atakayesongwa na matatizo ya ulimwengu yanayotokana na dhulma kiasi cha yeye aone kuwa anawajibika kufa kuliko kuendelea kuishi. Na Imam Husain ni mtu Mtukufu mno katika zama zake wala hana mfano popote duniani, kwa sababu nafsi yake tukufu ilikataa dhulma na unyonge akachagua kifo kuliko udhalili, na akawa kama alivyosema Ibn Nubatah, “Na Husain ndiye yule ambaye aliyaona mauti kuwa ni jambo tukufu katika maisha, na kuishi katika udhalili ni sawa na kifo.”
Nne: Husain a.s awe ni mtu wa kupigia mfano kutokana na ushujaa wake, uhodari wa msimamo wake, kutokana na tofauti kubwa iliyokuwa baina ya kikundi chake na jeshi la adui yake ambalo lilikuwa kubwa mno kwa idadi na maandalizi, kiasi ambacho sicha kulinganisha. Basi yafaa jambo hilo liwe la mazingatio kwa mwenye kuzingatia.
Tano: Imam Husain a.s pamoja na wote alikuwa nao miongoni mwa watu wa nyumba yake wote wawe ni kitambulisho cha mashujaa na kiigizo chema katika uvumilivu na ukarimu.
Sita: Athari ya Jihadi yake ibakie milele na mahali popote watu watakapokuwa wanagandamizwa na dhulma, basi uwe ni ukumbusho kwa kila yule ambaye ameitoa nafsi yake kwa ajili ya kuutumikia umma, asiizuwie nafsi yake kutoa uhai wake pindi kunapokuwa na maslahi katika mazingira yake.
Mwisho: Mimi nasema: “Ni mawaidha gani makubwa kuliko kufahamu kwamba, kila aliyeshiriki kumwaga damu ya Husain a.s. tayari Mwenyezi Mungu amekwishachukuwa kisasi chake, kwani huyo naye imma aliuawa au kufikwa na msiba mkubwa. Au ni Mazingatio gani makubwa zaidi (yanatakiwa) kuliko kuwa kaburi la Husain a.s ni eneo tukufu, wakati makaburi ya maadui zake ni mahala pa kutupia vinyesi vya wanyama na mengine yamefanywa kuwa machinjioni?
“Je waliofanya maovu wanadhani kuwa tutawafanya kama wale walio amini na kutenda mema, ili kwamba uhai wao na mauti yao yawe sawa?
Ni hukumu mbaya kabisa wanayoihukumu” Qur’an 45:21
Kwa kumalizia naivamia meza ya washairi ili nisome beti kadhaa kutoka ndani kabisa ya moyo wangu japo kwa ufupi ni msemeshe Imam huyu shujaa.
Ewe mjukuu wa Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, utajo wako ni mzuri nawe umetukuka mno kwa utajo huo na kwa fahari hiyo huna mfano wake.
Ewe Mjukuu wa Mjumbe wa Mwenyezi Mungu moyo wangu umejaa utajo wako
Ni nani atakayeweza kudhibiti mambo yako mema, kwani kila jambo jema hiyo ndiyo tabia yako ewe mwezi wenye nuru.
Ewe Mjukuu wa Mjumbe wa Mwenyezi Mungu mimi niko kwenye uongofu aliotuongoza Ahmad Babu yako mwema.
Amani iwe juu yako asubuhi na jioni ulimwengu unakutakia, na wadudu pia wanazisambaza salamu.