Change Language: English

UONGO NA MISIMAMO

UONGO KUHUSU KUONGEZEKA RIZIKI NA KUPAKA WANJA SIKU YA ASHURA Hadithi nyingi za uongo zilizushwa na kunasibishwa na Mtakasifu Mtume (s) kuhusu fadhila ya siku ya Ashura. Hadithi hizo kiini chake ni: fadhila kwa kuwafanyia familia yako karamu katika siku hiyo, kupaka wanja, mafuta na manukato na kujipamba…!! Hadithi zote hizo ni dhaifu katika sanadi na nasi yazo ni ‘gharibu’. Ulamaa wa Sunni wametamka wazi kwamba hizo hadithi ni katika uzushi wa watu wajinga katika Ahlu Sunna, na kwamba ni uzushi wa waongo (kama alivyosema Al-Ayniy) na kwamba zina uongo ambao unaosisimua ngozi (kama alivyosema Ibnul Jawzi), na kwamba ni uzushi wa wauaji wa Imam Husayn (a)- Bani Umayyah, Mwenyezi Mungu awalaani- (kama anavyosema Al Hakim na wengine). Kwa ubainifu huu wa ulamaa hawa wakubwa unatuondolea kazi ya kuchunguza sanadi ya hadithi hizo za uzushi. Hapa hizi ni baadhi ya hadithi hizo na baadae tutatoa msimamo wa ulamaa wa Kisunni: i. As-Shawkaniy: ‘Yeyote atakayewafanyia wasaa familia yake siku ya Ashura, basi Allah atamfanyia wasaa mwaka mzima.’ Imepokelewa na At-Twabraniy kutoka kwa Anas, ‘marfuu’. Katika sanadi yake kuna Al Hayswam bin Shadaakh ambae ni ‘majhuli.’ Pia ameipokea Al-‘Akiliy kutoka kwa Abu Hurayra na akasema Sulayman bin Abi Abdillah ni majhuli na hadithi ‘ghayr mahfudh’. ii. Na akasema katika Tamko la Ibnul Jawziy قال ابن الجوزي في ( الموضوعات ) ج2 ص 112 : " قد تمذهب قوم من الجهال بمذهب أهل السنة فقصدوا غيظ الرافضة فوضعوا أحاديث في فضل عاشوراء ونحن براء من الفريقين ، وقد صح أن رسول الله ( ص ) أمر بصوم عاشوراء إذ قال : إنه كفارة سنة ، فلم يقنعوا بذلك حتى أطالوا وأعرضوا وترقوا في الكذب " . Ibnul Jawzy katika kitabu chake ‘Al-Mawdhuuaat’( الموضوعات ) Juz. 2, uk. 112, anaandika: Wako baadhi ya majahili ambao wamejitia katika madhehebu ya Ahl Sunnah na wakalenga kuwaudhi ma-Rafidha (ma-Shia), na kwa sababu hiyo wakazusha hadithi kuhusu utukufu wa Ashura. Hakika sisi tuko kando na makundi yote mawili. Imesihi kwamba Mtume (s) aliamrisha kufunga siku ya Ashura pindi aliposema kwamba ni ‘kafara ya mwaka mzima’ Ibnul Jawziy:…miongoni mwa hadithi ambazo walizizusha… “imepokewa kutoka kwa A’raji kutoka kwa Abu Hurayra, alisema: Mtume (s) alisema: Hakika Allah aliwafaradhisha Bani Israil saumu ya siku moja katika mwaka, nayo ni Ashura ambayo ni siku ya kumi ya mwezi wa Muharram, kwa hiyo ifungeni na wafanyieni wepesi (karamu) ahli zenu (familia), kwani atakayefanya wepesi kwa familia yake kwa mali yake siku hiyo, basi Mwenyezi Mungu atamfanyia wepesi siku zilizobaki za mwaka wake. Basi mfunge siku hiyo kwani ni siku Mwenyezi Mungu alikubali toba ya Adam (a), na ni siku ambayo Mwenyezi Mungu alimpandisha ndani yake Idris (a) daraja ya juu, na ni siku ambayo Mwenyezi Mungu alimuokoa Ibrahim (a) na moto, na ni siku ambayo Nuhu (a) aliteremka kutoka katika safina, na ni siku ambayo Mwenyezi Mungu aliteremsha ndani yake Tawrat kwa Musa (a), na kumfidia Ismail (a) na kuchinjwa, na ni siku ambayo Mwenyezi Mungu alimtoa Yusuf (a) kutoka ndani ya jela, na ni siku ambayo Mwenyezi Mungu alimrudishia Ya’qub macho yake kuona, na ni siku ambayo Mwenyezi Mungu alimuondolea Ayub (a) maradhi yake, na ni siku ambayo Mwenyezi Mungu alimtoa Yunus (a) kutoka katika tumbo la papa, na ni siku ambayo Mwenyezi Mungu alipasua bahari kwa Bani Israil, na ni siku ambayo Mwenyezi Mungu alimsamehe Muhammad (s) dhambi yake, iliyotangulia na ya baadae, na ni siku ambayo Musa (a) alivuka salama bahari. Na katika siku hii, Mwenyezi Mungu aliteremsha toba yake kwa watu wa Yunus (a), kwa hiyo basi yeyote atakayefunga siku hii atapewa kafara ya miaka arobaini. Pia siku ya mwanzo iliyoumbwa na Mwenyezi Mungu ni Ashura…na mvua ya kwanza iliyoteremka ni siku ya Ashura, na rehema ya kwanza iliyoteremka ni siku ya Ashura, yeyote atakayefunga siku ya Ashura ni sawa na mtu aliyefunga zama zote, na ni saumu ya mitume… na yeyote atakayehuisha usiku wa Ashura ni sawa sawa na mtu aliyemuabudu Mwenyezi Mungu mfano wa ibada ya viumbe wa mbingu saba, na yeyote atakayeswali rakaa nne na akasoma katika kila rakaa Alhamdu mara moja na Qulhuwallahu mara hamsini, basi Mwenyezi Mungu atamsamehe miaka yake hamsini iliyopita, na miaka hamsini ijayo, na Mwenyezi Mungu atamjengea katika (daraja ya) malaika wa enzi ya juu mimbari milioni moja za nuru, na yeyote atakayenywesha nywesho la maji ni sawa na kwamba hajawahi kumuasi Mwenyezi Mungu hata chembe, na yeyote atakayelisha watu wa nyumba ambao ni maskini siku ya Ashura basi atapita kwenye Sirat kama vile umeme wa radi, na yeyote atakayetoa sadaka siku ya Ashura ni kama vile hajawahi kumrudisha anayeomba, na yeyote atakayeoga siku ya Ashura kamwe hatauguwa maradhi ila maradhi ya mauti, na yeyote atakayepaka wanja siku ya Ashura kamwe macho yake hayatauguwa (magonjwa ya macho) mwaka huo mzima, na yeyote atakayempapasa yatima kichwa chake ni kama vile amewafanyia wema yatima wote wa kizazi cha Adam (a). Na yeyote afungae siku ya Ashura, basi hulipwa thawabu za mahujaji elfu moja waliofanya umra, na yeyote atakayefunga siku ya Ashura, atapewa thawabu za mashahidi elfu moja, na atakayefunga siku ya Ashura ataandikiwa thawabu za mbingu saba, na ndani ya siku hiyo Mwenyezi Mungu aliumba mbingu na ardhi na milima na bahari na akaumba Arshi pia siku hiyo… na katika siku hiyo: akaumba Qalamu, lawhu, na Jibrilu (a), na akampandisha Isa (a), na akapewa Sulayman (a) ufalme. Na siku ya kiyama ni siku ya Ashura, na atakayezuru mgonjwa katika siku ya Ashura ni kana kwamba amezuru wagonjwa wote wa kizazi cha Adam.